
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia askari wawili wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha Lugalo Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji. Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Elias Kalinga, alithibitisha kuwa jeshi hilo linawashikilia askari hao wanaodaiwa kumpiga Siwetu Fundikira (45) hadi kusababisha kifo chake. “Kweli tunawashikilia askari wawili wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za kusababisha kifo cha raia mmoja juzi usiku, tunaendelea kuwahoji ili kubaini ukweli ili wafikishwe mbele ya sheria,” alisema Kamanda Kalinga. Aliwataja askari hao kuwa ni Sajenti Rhoda Robert na mume wake Koplo Ali Ngumbe wakazi wa Lugalo.
Kamanda Kalinga alisema juzi usiku majira ya saa saba usiku maeneo ya Manyanya, Wilaya ya Kinondoni, askari hao wanadaiwa kumpiga Fundikira ambaye inadaiwa alikwaruza gari lililokuwa likiendeshwa na watuhumiwa. Alibainisha kuwa baada ya magari hayo kukwaruzana, kulizuka vurumai iliyoambatana na kurushiana maneno ambayo mwisho wake ilikuwa ni kipigo.. “Askari hawa ni mtu na mke wake, tunawashikilia baada ya gari dogo walilokuwa wakitumia lenye namba za usajili T 880 AVW kukwaruzwa… wakaamua kushuka na kumpiga Fundikira na kumsababishia maumivu makali, ushahidi tulionao unaonyesha kulikuwa na fujo katika eneo lile na askari hao walidai walitukanwa,” alisema Kamanda Kalinga. Alisema baada ya kutembeza kipigo hicho, askari hao waliamua kumpakia Fundikira kwenye gari lao na kumkimbiza Kituo cha Polisi Salender..
“Watuhumiwa baada ya kuona hali ya Fundikira ikiwa mbaya kutokana na kipigo walichompa, waliamua kumpakia kwenye gari lao na kumkimbiza pale Salender, lakini wakati wanamfikisha hali yake ilikuwa mbaya mno na askari wetu wakawaweka chini ya ulinzi. “Polisi walimchukua Fundikira na kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alipelekwa moja kwa moja chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), lakini tayari alikuwa amekufa,” alisema.
Kamanda Kalinga aliongeza kuwa mbali ya askari hao, Jeshi la Polisi linamtafuta askari mwingine Private Mohamed Ngumbe ambaye alitoweka baada ya tukio hilo. “Bado tunamtafuta Private Ngumbe ambaye alitoweka mara baada ya tukio hili… uchunguzi wetu unaonyesha watu hawa wote ni ndugu,” alisema Kamanda Kalinga.
No comments:
Post a Comment